0
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Ally Hapi ameahidi kumaliza migogoro yote ya ardhi inayowakabili wananchi wa wilaya hiyo, ili wananchi waishi kwa amani na kupata muda wa kufanya shughuli za maendeleo na ikiwezekana maeneo mengine nchini yajifunze utatuzi wa migogoro ya ardhi kutoka Kinondoni.

Bw. Hapi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa mtaa wa Nyakasangwe kata ya Wazo wilayani humo, muda mfupi kabla ya kuzindua zoezi la upimaji wa ardhi na uwekaji wa bikon, kufuatia kumalizika kwa mgogoro wa kugombea ardhi uliokuwa ukiwakabili wananchi wa mtaa huo kwa kipindi kirefu.

Kadiri ya watu kumi walipoteza maisha kwenye mgogoro huo mwaka 2012 kutokana na mzozo baina ya wamiliki wa mashamba na wakazi waliodaiwa kuwa ni wavamizi wa maeneo, ambapo baada ya pande zinazohusika na mgogoro kufikia muafaka, eneo hilo limeanza kupimwa ili kila mwananchi apate haki yake, huku maeneo mengine ya huduma za kijamii pamoja na yale ya kibiashara na uwekezaji nayo yakihusishwa kwenye mradi huo.

Awali uongozi wa serikali ya Mtaa, Kamati mbalimbali za wakazi waliohusika kwenye mgogoro huo hadi ufumbuzi ulipopatikana pamoja na wawakilishi wa Kampuni ya Afro Map Ltd inayofanya kazi ya upimaji, walieleza hatua walizofikia hadi sasa na kutoa matumaini mapya kwa wananchi wa eneo hilo.

Post a Comment

 
Top