0
Wanaharakati watatu wa haki za binadamu nchini Burundi wamehukumiwa jela miaka 10 kwa kutishia usalama wa taifa hilo.

Wakati wakipewa hukumu hiyo wanaharakati hao Emmanuel Nshimirimana, Aime Constant Gatore na Marius Nizigiyimana hawakuwa Mahakamani.

Wanaharakati hao walikamatwa mwezi Juni mwaka 2017 wakiwa na nyaraka za maandalizi ya kongamano la wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo.

Viongozi wa Mashtaka walitaka wanaharakati hao kupewa kifungo cha kati ya miaka 20 hadi 25 kwa kosa ambalo wanasema watatu hao walipanga tukio la kuharibu amani.

Majaji katika Mahakama ya Muramvya, katikati ya nchi hiyo, walitangaza hukumu hiyo hata bila ya kuwepo kwa Mawakili wa wanaharakati hao.

Mwanaharaati maarufu nchini humo Gabriel Rufyiri, amelaani hukumu hiyo na kusema kwa mara ya kwanza, wanaharakati nchini humo wamepewa kifungo cha njia zisizoeleweka.

Hukumu hii imekuja wakati huu rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza akiendelea na kampeni ya kuibadilisha Katiba ili kuendelea kuongoza nchi hiyo kutoka Afrika ya Kati.

Serikali ya Bujumbura, imeendelea kushtumiwa na Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi kwa kukiuka haki za binadamu nchini humo na kuminya uhuru wa kujiueleza.

Post a Comment

 
Top