VURUMAI kubwa na taharuki imetokea jana katika chumba cha kuhifadhi
maiti katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi baada ya
ndugu wa marehemu Mathias Madega, kukabidhiwa maiti ambayo siyo ya ndugu
yao.
Hali hiyo ilitokana na watumishi wa afya kuuchukua mwili wa ndugu yao
huyo na kuwakabidhi watumishi wa Manispaa na kwenda kuuzika kwa madai
kuwa haukuwa na ndugu.
Tukio hilo lililovutia hisia za watu wengi wa mji wa Mpanda, lilitokea
saa 8:00 mchana baada ya ndugu wa Madega kufika katika chumba cha
kuhifadhi maiti kwa lengo la kuuchukua mwili wa mpendwa wao kwa ajili ya
maziko kulingana na taratibu za familia yao.
Baada ya wafiwa wakiongozwa na baba mdogo wa marehemu, George Madega,
kufika katika hoaspitali hiyo, walimkuta muuguzi ambaye waliongozana
naye mpaka chumba cha kuhifadhi maiti kisha akawaonyesha maiti moja
iliyokuwamo akidai kuwa ni ya ndugu yao hivyo wachukue kwa maziko.
Maiti waliyoifuata, ilikuwa imehifadhiwa kwa siku mbili, lakini maiti
waliyoonyeshwa, ilikuwa imeharibika vibaya na kutoa harufu kali
ikiashiria ni ya siku nyingi.
Majokofu ya chumba cha hifadhi ya maiti katika hospitali hiyo yameharibika.
Hata hivyo, baada ya kuifanyia ukaguzi maiti ile, walibaini kuwa si ya
ndugu yao, kitendo kilichowakasirisha na kumujia juu muuguzi ambaye
baada ya kuwaonyesha mwili huo, alirudi nje kukwepa harufu.
Muuguzi huyo aliwaeleza wafiwa hao kuwa watumishi wa Manispaa,
walikwenda hospitali hapo na kuuchukua mwili wakidhani ni wa yule asiye
na ndugu na kwenda kuuzika.
Kwa msingi huo, wafiwa hao walibaini kuwa maiti iliyokwenda kuzikwa na watumishi wa Manispaa, ndiyo ya ndugu yao.
Ndipo walipoanza kufuata taratibu za kisheria na kisha mahakama ikatoa
kibali kwenda kufukua kaburi na kukuta aliyezikwa ni ndugu yao.
Wafiwa hao waliuchukua mwili huo na kwenda kuuzika kwa taratibu za familia yao.
Mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali hiyo, George Nsalamba, alisema siku ya tukio hakuwapo.
Nsalamba alisema kosa hilo la kuchanganya maiti lilifanywa na
aliowaachia funguo za chumba cha hifadhi ya maiti akimtaja muuguzi
aliyekwenda kusimamia utoaji wa maiti ya kwanza ambayo ilizikwa na
Manispaa.
Aidha, mazishi ya Madega yamepangwa kufanyika leo katika makaburi ya Misunkumilo Manispaa ya Mpanda.
Post a Comment