0
Katibu Tawala Mkoa (RAS) wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi alivyovamiwa, kupigwa kwenzi, kushikwa matiti, hadi zipu ya sketi yake kung’oka na kujeruhiwa wakati akisimamia uchaguzi wa meya na naibu wake wa Jiji la Dar es Salaam uliopaswa kufanyika Februari 27. 

Pia, alidai kugongwa kichwani na kupokonywa faili lililokuwa na ajenda ya uchaguzi. 

“Walinifuata mezani nilipokuwa wakitaka niendelee na uchaguzi, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alilivuta faili lililokuwa na mwongozo wa uchaguzi na katika tukio hilo niliwafahamu walionivamia kwa majina na wengine kwa sura,” alidai Mmbando. 
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Flontina Sumawe kutoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Mmbando alidai kuwa Februari 27 alipewa jukumu la kusimamia uchaguzi huo ambao ulipaswa kufanyika nyakati za saa nne asubuhi katika Ukumbi wa Karimjee. 
“Nikiwa Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam nilikuwa ni mwenyekiti wa uchaguzi huo, wajumbe wote walifika, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Salehe Yohana ambaye alikuwa Katibu alifungua uchaguzi huo kwa sababu kolamu ya wajumbe ilikuwa inajitosheleza,” alidai Mmbando. 
Alidai kikao kilifunguliwa, lakini katibu aliahirisha uchaguzi kwa sababu alipokea zuio la Mahakama la kuendelea na akawaarifu wajumbe. 

Mmbando aliendelea kudai kuwa baada ya kuahirishwa, wajumbe wa CCM walitoka nje, lakini wa vyama vingine wakiwamo Ukawa, walimvamia wakimtaka aendelee. 
Alidai watu wengine aliowatambua siku hiyo ni Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea ambaye alimuambia kuwa yeye ni kibaraka wa CCM, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara aliyekuwa akimsisitiza hakuna kuondoka bila kuendesha kikao. 
Akiendelea kutoa ushahidi mahakamani hapo, Mmbando alidai Diwani wa Kimanga, Manase Mjema (56) alimuona akiwatuliza wenzake na kuwataka wamuachie.
Mmbando alidai aliokolewa na polisi na wafanyakazi wa jiji kupitia mlango wa nyuma. Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 8, atakapoendelea kusikiliza ushahidi.

Post a Comment

 
Top