Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Safari Bungate, miaka 51, mkazi wa
Usagara, wilayani Misungwi mkoani Mwanza ameuawa na kundi la watu kwa
kupigwa mawe na fimbo kwa madai ya kuiba kuku nyumbani kwa mtu.
Marehemu mara baada ya kupigwa mawe na kuuawa akiwa amefungiwa kuku aliyekamatwa naye
Taarifa ya jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza imesema kuwa tukio hilo
limetokea tarehe 26.01.2017 majira ya saa 10 usiku katika kijiji cha
Kanyelele, wakati mwenye nyumba bwana Tetema Mathias akiwa amelala na
familia yake.
Inadaiwa kuwa marehemu huyo alifika katika nyumba hiyo akaingia ndani
kupitia dirishani na kuiba kuku mmoja, ndipo wakati alipokuwa anataka
kuondoka mwenye nyumba huyo alimuona na kuanza kupiga yowe ya mwizi
akiomba majirani wamsaidie kumkamata huku akimkibiza barabarani.
Inasemekana kuwa majirani waliamka na kufanikiwa kumkamata marehemu
akiwa na kuku amemshikilia kisha wakaanza kumpiga kwa mawe na fimbo
sehemu mbalimbali za mwili wake kitendo kilichopelekea marehemu
kupoteza fahamu na baada ya muda mchache alifariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi amesema kuwa raia wema
walitoa taarifa polisi ndipo askari walifika eneo la tukio na kukuta
mtuhumiwa wa wizi akiwa tayari amefariki dunia.
Amesema mwili wa marehemu tayari umefanyiwa uchunguzi na daktari na
kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi na kwamba mwenye
nyumba Bwana Tetema Mathias anashikiliwa na jeshi la polisi kwa
mahojiano zaidi
Post a Comment