0
KATIKA hali ya kushangaza, juzi Jumatano kiungo mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa alijikuta katika wakati mgumu kufuatia begi lake kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Tukio hilo limetokea kwa kiungo huyo alipokuwa sambamba na wachezaji wengine wa timu hiyo wakitokea Zanzibar katika michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kutolewa katika mchezo wa nusu fainali kwa penalti 4-2 dhidi ya Simba. Gazeti hili lilishuhudia Mzambia huyo akihaha kulitafuta begi hilo akiwa na Wazimbabwe, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko.

Chirwa ambaye hakufanikiwa kucheza mchezo hata mmoja wa michuano hiyo, alikuwa akilalamika kwamba begi lake aliliweka pamoja na mizigo mingine ya wachezaji wa timu hiyo, lakini anashangaa halioni. Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh akaamua kuingilia kati na kufuatilia kwa zaidi ya dakika 20, lakini jitihada zao hazikuzaa matunda mpaka wanaondoka bandarini hapo.

“Begi langu, la Chirwa na la Kamusoka tuliweka pamoja na vifaa vingine humu lakini sasa tumefika hapa tunashangaa hatulioni, sasa litakuwa limeenda wapi,” alisikika Ngoma alipokuwa akiongea na meneja wa timu hiyo huku Chirwa akisisitiza kuwa alitoka nalo hotelini mpaka bandarini kabla ya kupanda boti na kurejea Dar.

Hafidh aliliambia gazeti hili kuwa, baada ya kuona muda unakwenda na halionekani, aliamua kuacha maagizo bandarini hapo ili litafutwe na likipatikana wapewe.

Post a Comment

 
Top