OFISI ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimwa Kusini, Kata ya Ipagala, Manispaa
ya Dodoma imefungwa na watu wasiojulikana na kusababisha mwenyekiti wake
Ismail Seif kufanya kazi zake akiwa nyumbani kwake.
Tukio hilo lilitokea siku moja baada ya kufanyika mkutano wa hadhara wa
wakazi wa eneo hilo uliokuwa na lengo la kuwasomea wananchi mapato na
matumizi kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba na Desemba.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimwa, Ismail Seif
alisema mkutano huo ulifanyika wiki iliyopita baada ya kuitishwa na
wananchi kwa mujibu wa kalenda za mikutano ya mitaa.
“Siku iliyofuata yaani Jumapili asubuhi nilikuta ofisi yangu ikiwa
imevunjwa kufuli na kuwekwa kufuli lingine ambalo ni jipya na watu
waliofanya hivyo mpaka sasa bado hawajafahamika,” alisema.
Seif alisema kutokana na ofisi hiyo kufungwa sasa analazimika kufanya
shughuli zake nyumbani mpaka hapo Ofisi ya Mtendaji kwa kushirikiana na
polisi watakapoamua kuvunja kama vifaa vyote vipo au kuna uharibifu
uliofanyika.
Alisema tayari taarifa ya kuvunjwa kwa kufuli la ofisi na kuwekwa jipya
ameshapeleka ofisini kwa mtendaji wa kata pamoja na Kituo cha Kati cha
Polisi na kupatiwa RB namba Dom/RB/318/2017. Ofisa Mtendaji wa Kata ya
Ipagala, Manispaa ya Dodoma, Khalifa Malaja alikiri kupokea taarifa za
tukio hilo.
Alisema taarifa ya mwenyekiti huyo aliipata siku moja baada ya kufanyika
mkutano ambao hata hivyo ulionekana kuwa na viashiria vya kukosa amani.
Post a Comment