UPATIKANAJI
wa nafasi za ajira 600 za udereva zilizotangazwa na Kiwanda cha Saruji
cha Dangote cha Mtwara hivi karibuni, umegubikwa na tuhuma za rushwa
baada ya baadhi ya madereva walioziomba kudai kutakiwa kutoa 'kitu
kidogo' ili waitwe kwenye usaili.
Kutokana na changamoto hiyo, baadhi ya madereva wasio na uzoefu wa
kuendesha malori ya mizigo, wakiwamo madereva wa daladala hasa za Dar es
Salaam, wanadaiwa 'kulamba' ajira hizo na kuzua hofu ya usalama wa
malori hayo.
Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) Makamo Makuu Dar es Salaam, Mussa Misalaba aliiambia
Nipashe jana kuwa wanazo taarifa hizo na wanazifuatilia.
"Hilo suala tunalifahamu na tunaendelea kulifanyia kazi," alisema Misalaba. "Kwa hiyo ndiyo 'in short' hiyo (kwa kifupi)."
Desemba 16, mwaka jana, uongozi wa kiwanda hicho kikubwa zaidi katika
uzalishaji wa saruji kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki, kilitangaza
nafasi za ajira kwa madereva 594 wenye uzoefu wa magari makubwa ya
mizigo.
Kwa mujibu wa tangazo hilo lililochapishwa pia kwenye gazeti hili siku
hiyo, nafasi hizo zinawahusu Watanzania wenye umri kuanzia miaka 26 hadi
55 wenye uzoefu wa miaka isiyopungua mitano katika kuendesha magari
makubwa ya mizigo na leseni ya Daraja E.
Kiwanda hicho kilichopo mkoani Mtwara, kilitangaza ajira hizo ikiwa ni
siku chache baada ya mmiliki wake, tajiri namba moja barani Afrika,
Alhaji Aliko Dangote, kuleta malori 600 nchini kwa ajili ya kusafirishia
bidhaa zake.
Mfanyabiashara huyo alitua nchini na kuzugumza na Rais John Magufuli na
kubainisha kuwa mradi wake ambao ulisimama mwishoni mwa mwaka jana hauna
tatizo isipokuwa uliingiliwa na wapiga 'dili' ambao Rais Magufuli
aliahidi atawashughulikia.
Lakini sasa kiwanda hicho kikianza tena uzalishaji wa saruji baada ya
kusimama kwa wiki kadhaa kutokana na changamoto za kiuendeshaji,
utaratibu unaoendelea wa kuajiri madereva 594 umedaiwa kugubikwa na
vitendo vya rushwa.
Baadhi ya madereva walioomba ajira hizo wamedai kutakiwa kutoa kati ya
Sh. 300,000 na 500,000 ili waitwe kwenye usaili na kupewa ajira hizo.
"Ajira hizi kuzipata lazima uwe na pesa ya kuwapa wanaosimamia zoezi
lenye la kutoa ajira. Niko hapa Mtwara kwa wiki mbili sasa nasubiria
ajira. Nilitoka Dar Desemba 27 lakini nilipofika hapa nikaambiwa bila
kutoa lati tatu (Sh. 300,000), siwezi kuitwa hata kwenye 'interview'
(usaili)," alisema mmoja wa madereva walioomba ajira hizo.
Dereva mwingine aliyetoka Dar es Salaam kwenda Dangote kufuatilia ajira
hizo za udereva wa malori, aliiambia Nipashe juzi kuwa wanaosimamia
ajira hizo wamekuwa wakiwataka kurushwa.
"Mimi nipo hapa Mtwara tangu wiki iliyopita. Nimekidhi vigezo vyote
lakini wanataka niwape laki tano (Sh. 500,000) ili kupewa ajira. Nipo
hapa Dangote nasubiri," dereva huyo alisema na kuongeza:
"Kuna madereva nawafahamu wana uzoefu wa kuendesha daladala za Dar es
Salaam lakini nimewakuta hapa na wamelamba ajira za kuendesha magari
makubwa ya mizigo."
Akiwa karibu na eneo la kiwanda hicho jana mchana, dereva mwingine wa
malori makubwa aliyeomba ajira hizo, alidai rushwa imekithiri katika
mchakato wa kusaka ajira hizo.
FUNGU JINGINE
Alidai kiwango cha chini ya kuwapa wanaoratibu ajira hizo ili uitwe
kwenye usaili ni Sh. 300,000 lakini kuna fungu jingine ambalo linapaswa
kutolewa kwa wanaowafanyia usaili madereva wanapokabidhiwa gari ili
kuangalia uwezo wao.
"Kima cha chini ni Sh. 300,000 ambazo unatakiwa kuwapa hawa jamaa ndipo
uitwe katika usaili. Wale wanaofanya usaili, hawapokei fedha moja kwa
moja. Si unajua tena watu wa PCCB (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa - Takukuru) wanaogopa," alisema mkazi huyo wa Dar es Salaam
akifafanua zaidi jinsi mchezo huo mchafu unavyofanyika.
"Unampa mtu kwa mkono, anampelekea mhusika, yaani upande wa wale wanaoajiri. Akishapokea chake, unaitwa kwenye usaili.
"Ukishapita usaili wa kwanza, kuna usaili wa pili ambao ni kukabidhiwa
gari uendeshe. Nako ukifanya vibaya kama huna uzoefu sana wa magari
makubwa, unatoa laki moja (Sh. 100,000) hadi lakini mbili (Sh.
200,000)."
Alisema yeye na madereva wengine wengi walioomba kazi hiyo, walituma
maombi kwa njia ya Posta lakini walipoona wanakaa muda mrefu bila kuitwa
kwenye usaili, waliamua kusafiri kwenda Mtwara, kilipo kiwanda hicho.
"Mimi bado nipo hapa Mtwara. Tupo maelfu. Kila siku kuna mamia ya madereva wanaingia hapa kusaka bahati yao.
"Kwa wiki moja sasa nipo hapa naona watu karibu 200 kila siku wanafika
hapa kuomba ajira za udereva. Watu wanalala katika mabanda ya mama lishe
maana hata nyumba za kulala wageni hazitutoshi kwa sasa," alisema zaidi
dereva huyo.
Aliongeza kuwa madereva wengi wamechangamkia fursa hizo za ajira kwa
kuwa wakishapata kazi, watakuwa na uhakika wa ajira ya uhakika na fursa
zingine ikiwamo mikopo.
Mwenyekiti wa wenyeviti wa vijiji jirani na kiwanda hicho, Rashid
Abdelleman, alikiri kupokea malalamiko ya madereva kuomba kutoa 'kidogo'
ili wapate nafasi za ajira kwenye kiwanda hicho.
Abdelleman ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Naumbu Kusini,
alisema: "Madereva wanalalamika kwamba wanaambiwa watoe laki tatu ili
wapenye kwenye usaili. Agizo la hivi karibuni la Rais Magufuli
limefanikiwa kuondoa watu wa kati. Kulikuwa na kampuni za ajira hapa,
sasa hazipo tena, lakini rushwa inaendelea. Unashaangaa kiwanda kipo
hapa Mtwara lakini hata mtunza maua anatoka Arusha."
MALORI KUANGUSHWA
Akizungumzia kuhusu tuhuma hizo, mmoja wa watendaji wa Kiwanda cha
Safuri Dangote ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa kuwa si
msemaji wa kiwanda hicho, alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo katika
utoaji wa ajira na kutahadharisha kuwa madereva wasiokuwa na uzoefu
waliopewa ajira kwa kupitia mlango wa nyuma wanaweza kuwa hatari kwa
malori yao.
Alisema tayari uongozi wa juu wa kiwanda umearifiwa kuhusu
kinachoendelea juu ya ajira hizo na huenda mchakato ukasitishwa na
kurudiwa upya chini ya usimamizi maalum wa serikali ili kuepuka rushwa.
"Ni kweli tumepata malalamiko hayo lakini wa kulizungumzia zaidi hili ni
'CEO' (Ofisi Mtendaji Mkuu) wa Kiwanda cha Dangote, Harpreet Duggal.
Yeye (Duggal) ndiye msemaji wa kiwanda," alisema mtendaji huyo na
kuongeza:
"Inasemekana baadhi ya madereva wanaopitishwa kupatiwa ajira hizo si
wazoefu. Unaangalia uwezekano ili mchakato usimamie na urudiwe. Wawapo
wakaguzi maalumu ili kuepuka hao wanaopita kwa rushwa.
"Kwa maelezo niliyopata, wanashirikiana baadhi ya watendaji wa kiwanda
wanaohusika na hizo ajira lakini wao hawachukui pesa kutoka kwa dereva
moja kwa moja. Kuna watu maalum wanaopokea pesa hizo, wako nje ya
kiwanda, wakishapokea fungu, wanachukua jina la aliyetoa kisha anaitwa
kwenye usaili.
"Nasikia pia sehemu kubwa ya madereva waliochukuliwa hadi sasa ni
madereva wa daladala. Ni hatari sana kwa magari yetu, wasituharibie
kazi. Rais Magufuli ametusaidia kuondoa watu wa kati lakini tunaendelea
kuhujumiana sisi wenyewe."
Alipokutana na Alhaji Dangote Ikulu jijini Dar es Salaam Desemba 10,
mwaka jana, Rais Magufuli alimwahidi bilionea huyo kuwa serikali
itawaondoa wapiga dili wote waliokuwa wanakamishwa mradi huo wenye
thamani ya dola za Marekani milioni 600 (zaidi ya Sh. trilioni 1.2).
"Tatizo la Watanzania ni watu wa katikati. Hapakuwa na tatizo (kwenye
mradi wa Dangote) lakini pamekuwapo watu wapiga dili kwenye mradi huu,
badala ya kununua gesi moja kwa moja TPDC (Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania) ambacho ni chombo cha serikali, anaingia mtu katikati
pale anataka naye atengeneze kamisheni," alisema Magufuli.
"Tunataka eneo kwa ajili ya gati (bandari) kaeneo kadogo tu pale, watu
wanataka wakalipwe Sh. bilioni 43 (bandari ya kiwanda cha Dangote
Mtwara) kana kwamba watu wanachukua maeneo kule ili wakalipwe fidia.
Kwa hiyo wapiga dili ndio walikuwa wameuingilia huu mradi na sasa hivi
wameshindwa na watalegea moja kwa moja kwa sababu Dangote wamemwona
mwenyewe yuko hapa na mwezi huu analeta magari 600 na yameshaanza kuja
kwa ajili ya kubeba simenti na amezungumza, ninyi wenyewe mmemsikia."
Post a Comment